Kiungo Khalid Aucho huenda akaendelea kuwa nje kwa wiki kadhaa baada ya kutonesha majeraha alipokuwa na timu ya Taifa ya Uganda
Licha ya kocha Milutin Micho kumjumuisha Aucho katika kikosi chake kwa ajili ya michezo ya kirafiki katika kalenda ya FIFA, nyota huyo hakuweza kushiriki mchezo wowote baada ya kutonesha majeraha
Micho alithibitisha kuwa Aucho alikuwa akisumbuliwa na tatizo la misuli hivyo asingeweza kumtumia
Akizungumza baada ya mchezo wa kirafiki dhidi ya Mafunzo Fc jana, kocha msaidizi wa Yanga Cedric Kaze alisema walimruhusu Aucho kujiunga na timu ya Taifa kwa kuwa afya yake ilikuwa imeimarika
Amesema wanasubiri atakaporejea kubaini ukubwa wa jeraha alilopata na kumpa matibabu stahiki
"Ni kweli tulimruhusu Aucho kwenda kujiunga na timu ya Taifa baada ya afya yake kuwa imeimarika, lakini tumepata taarifa kuwa ametonesha jeraha akiwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa, kesho atarejea nchini na kufanyiwa vipimo ili kujua ukubwa wa tatizo lake," alisema Kaze
Huenda Aucho ataukosa mchezo wa ligi kuu unaofuata dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa April 06 akiungana na Feisal Salum 'Fei Toto' ambaye pia aliumia akiwa kwenye majukumu ya timu ya Taifa ya Tanzania