Huko mtaani utawasikia Wananchi wanalalamika kuwa kukaa wiki mbili pasipo kuiona timu yao ikicheza ni jambo gumu! Wenyewe si wamezoeshwa kutetema na Fiston Mayele kila wiki!
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema huenda wakacheza mechi kadhaa za kirafiki ili kuendelea kukiweka kikosi katika hali ya ushindani
Yanga tayari imerejea kambini kuanza maandalizi ya mchezo dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa April 06, uwanja wa Azam Complex, ingawa ziko taarifa kuwa Azam Fc wanaweza kuurudisha mchezo huo katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Bumbuli amesema michezo hiyo itategemea na mapendekezo ya benchi la ufundi na upatikanaji wa klabu hizo
"Ndio wiki mbili ni nyingi sana, upo uwezekano tutacheza mechi kadhaa za kirafiki ili kuhakikisha wachezaji wanabaki katika hali ya ushindani kama wenzao ambao wameitwa timu za Taifa. Nafikiri kwenye siku chache hizi tutatangaza tutacheza na nani," alisema Bumbuli
Akizungumzia mchezo unaofuata dhidi ya Azam Fc, Bumbuli amesema wamejipanga kuhakikisha wanaondoka na alama zote tatu
"Hawa Azam Fc ni mongoni mwa zile timu ambazo tuliambiwa zinatumika kutuzuia tusiwe mabingwa, sasa tunajipanga kwelikweli kuhakikisha tunawafunga. Sisi hatuchagui uwanja, iwe Azam Complex, uwanja tuliouzoea sana au walete hata Benjamin Mkapa sisi tuko tayari," alitamba Bumbuli