Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, ameanza kupiga hesabu nzito za kuvuna pointi sita katika michezo miwili iliyombele yao dhidi ya Azam FC na Simba, ambayo anaichukulia kama fainali kwao kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara
Yanga inayoongoza ligi hiyo ikiwa na pointi 48, huku ikiwa na kibarua dhidi ya Azam FC mchezo utakaopigwa Aprili 6, katika Uwanja wa Azam Complex ulioko Chamazi, Dar es Salaam na baada ya hapo itakutana na Simba Aprili 30, mwaka huu.
Nabi ameendelea kusisitiza kuwa kila mchezo kwao ni fainali lakini michezo hiyo miwili ni migumu zaidi hasa kulingana na ubora wa timu hizo.
Alisema licha ya kupata matokeo mazuri katika michezo yao 18, hawako katika ubora sana wakuweza kuwafanya kuwabeza wapinzani wao, hivyo wanapaswa kuwaheshimu ili kuhakikisha wanapata pointi katika mechi hizo
"Hizi ni mechi ngumu kuna Azam FC na Simba hasa ukizingatia ni 'Derby', ndio kubwa kwa Afrika na huchukuliwa kwa umuhimu hali ambayo kila mmoja anahitaji kupata pointi kufikia malengo yake," alisema Nabi
Alisema anaamini mechi hizo ni muhimu kuanza kujipanga mapema ili kuhakikisha wanaweka mikakati yao imara
Baada ya mchezo dhidi ya Azam Fc April 06, Yanga itakuwa na takribani wiki tatu kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba ambao utapigwa April 30 katika uwanja wa Benjamin Mkapa Yanga ikiwa mwenyeji wa mchezo huo
Huo utakuwa mchezo wa tatu kwa Yanga na Simba kukutana msimu huu baada ya mchezo wa Ngao ya Jamii ambao Yanga ilishinda bao 1-0 na mchezo wa ligi duru ya kwanza uliomalizika kwa suluhu ya bila kufungana