Hivi karibuni Mwenyekiti wa zamani wa klabu ya Simba Ismail Aden Rage alinukuliwa na gazeti moja la kila siku akidai kuwa Yanga haiwezi kuchukua ubingwa wa ligi kuu licha ya kuongoza kwani zipo mechi hawataweza kushinda
Rage alizitaja mechi hizo kuwa ni dhidi ya KMC, Azam Fc, Simba, Namungo na Mbeya City
Tayari Yanga imechukua alama tatu dhidi ya KMC huku ikijipanga kushinda mchezo unaofuata dhidi ya Azam Fc
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema kauli ya Rage imewaongezea 'mzuka' na watahakikisha wanashinda mechi zote ikiwa ni pamoja na mechi zilizosalia katika 'mkeka' wa Rage
"Si alisema kwamba wana mechi nne wameziandaa ili kutukwamisha ikiwemo KMC, Azam, Simba na Namungo, kwa hiyo na sisi hiyo kauli tumeichukulia serious kabisa kwasababu amesema wamejiandaa, tumeshaanza na KMC tumeshapiga, tutaendeleza vipigo kwa kila anayekuja mbele yetu," alitamba Bumbuli
Mchezo dhidi ya Azam Fc utapigwa April 06 ligi itakaporejea baada ya kumalizika kwa mechi za Kimataifa
Yanga iko kileleni mwa msimamo wa ligi ikiwa na alama 48 baada ya kucheza mechi 18. Wako mbele kwa alama 11 dhidi ya Simba inayoshika nafasi ya pili
Wakati Rage akitaja michezo ya kuikwamisha Yanga, Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi yeye ana mkakati wa kushinda mechi zote tano zinazofuata ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kushinda ubingwa