Baada ya kukosekana uwanjani kwa takribani miezi mitatu kutokana na majeraha, mlinzi Kibwana Shomari sasa amerejea
Juzi katika mchezo wa kirafiki dhidi ya timu ya Taifa ya Somalia, Kibwana alicheza kwa takribani dakika 15 akichukua nafasi ya Djuma Shabani ambaye pia alirejea kikosini baada kupona ugonjwa wa malaria
Kurejea kwa Kibwana na wachezaji wengine waliokuwa majeruhi ni habari njema kwa Yanga katika ngwe hii ya lala salama ligi kuu ya NBC
Katika mchezo huo pia Wananchi walimshuhudia Mcongoman Chico Ushindi akianza na kufunga bao la kusawazisha kwa upande wa Yanga katika mchezo uliomalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1
Ushindi alishindwa kumaliza mchezo baada ya kupata majeraha mwanzoni mwa kipindi cha pili, hata hivyo imeelezwa hayakuwa majeraha makubwa na huenda akawa tayari kuikabili KMC siku ya Jumamosi
Walinzi Abdallah Shaibu 'Ninja' na David Bryson nao walikuwa sehemu ya wachezaji wa akiba ingawa hawakupata nafasi ya kucheza
Kocha Nasreddine Nabi aliwatumia Ibrahim Bacca na Dickson Job eneo la ulinzi wa kati akimpumzisha nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto wakati upande wa kushoto alimtumia Yassin Mustafa ambaye sasa yuko fiti kwa asilimia 100%
Wachezaji Khalid Aucho, Farid Mussa na Saido Ntibazonkiza walikosekana katika mchezo huo, Aucho na Farid wamepona majeraha wakati Saido bado yuko katika program ya kumuimarisha, akitarajiwa kukosekana kwa wiki moja zaidi