Mkurugenzi wa Uwekezaji GSM Injinia Hersi Said amesema ushirikiano wa Yanga na GSM Foundation pamoja na Taasisi ya Ali Kimara, wamefanikisha mchezo wa Kimataifa wa kirafiki kati ya Yanga dhidi ya timu ya Taifa ya Somalia ambao utapigwa keshokutwa Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Asilimia 40 ya mapato ya mchezo huo yatakwenda kuchangia Ali Kimara Foundation huku GSM wakiahidi kuchangia Tsh Milioni 10
"Ushirikiano kati ya Yanga Sc, Taasisi ya GSM na Taasisi ya Ali Kimara unakwenda kutuletea mchezo huu ambao Yanga wanakwenda kuchangia asilimia 40% ya mapato yatakayopatikana na sisi GSM tutatoa mchango wetu wa Shilingi Milioni 10 kwa ajili ya kwenda kusapoti Taasisi ya Ali Kimara," alisema Hersi
Nae Mtendaji Mkuu wa Yanga Senzo Mazingisa amesema klabu hiyo kwa kushirikiana na GSM Foundation, wataendelea na utaratibu wa kuwasaidia wale wenye uhitaji huku akiwahamasisha wengine kujitolea kuzisaidia jamii zao kadiri wanavyoweza
"Tumekuwa na Ushirikiano mzuri na GSM katika kurudisha kwenye Jamii na imekuwa sehemu ya Utamaduni wetu kokote tunapokwenda na Klabu yetu nchini, kuna mahitaji mengi sana kwenye Jamii yetu na tuna wajibu wa kuhakikisha tunawavutia na wengine ili tuwasaidie wale wenye uhitaji kwa chochote tulichojaliwa," alisema Senzo