Uongozi wa Yanga tayari umeanza mchakato wa kuwaongezea mikataba wachezaji wake ambao wanamaliza mikataba mwishoni mwa msimu
Miongoni mwa wachezaji hao ni kungo mshambuliaji Saido Ntibazonkiza ambaye msimu huu umekuwa mzuri sana kwake
Akiwa amefunga mabao sita na kutoa pasi tano za mabao katika mashindano yote, Ntibazonkiza amekuwa mchezaji mwenye thamani kubwa katika kikosi cha Yanga
Mwenyekiti wa Kamati ya Ufundi, Dominic Albinius amesema tayari wamefanya mazungumzo na Ntibazonkiza na atasaini mkataba mpya kuendelea kuwatumikia Wananchi
Albinus amesema kwa ubora alionao Saido, mashabiki hawawezi kuwaelewa viongozi kama hatapewa mkataba mpya haraka
"Hakuna ambaye anaweza kuthubutu kusema Saido asiongezewe mkataba kwa sasa. Ukisema usimpe mkataba wananchi si wanaweza kukutoa roho mara moja!"
"Tulipoongea naye ametuambia ana furaha ya kuwa katika familia hii na jina lake limekuwa na heshima zaidi hasa kwao amekuwa kila akirudi, anaagizwa jezi nyingi za Yanga kutoka kwa rafiki na wengine kuzinunua," Albinus amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
Pamoja na Saido wachezaji wengine ambao mikataba yao inamalizika mwishoni mwa msimu ni pamoja na nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto, Kibwana Shomari, Yassin Mustafa, Zawadi Mauya, Deus Kaseke na Farid Mussa
Albinus amesema wamedhamiria kuhuisha mapema mikataba ya wachezaji wote ambao kocha anawahitaji kuendelea kuwa nao msimu ujao ili kuhakikisha hakuna mchezaji anaondoka akiwa huru