Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema kesho wanaanza upya hesabu za ligi katika mchezo wa kwanza wa mzunguuko wa pili dhidi ya Kagera Sugar
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari kuelekea mchezo huo, Nabi amesema hawafikirii chochote walichofanya katika duru ya kwanza, wakidhamiria kupata matokeo mazuri katika mchezo huo
Nabi amesema duru ya pili itakuwa ngumu zaidi ya ilivyokuwa duru ya kwanza hivyo wachezaji wake wanahitaji kupambana kuhakikisha wanapata matokeo
"Tumejipanga vyema kuelekea mchezo dhidi ya Kagera Sugar, huu ni mchezo wa kwanza duru ya pili tunahitaji kushinda. Hatufikirii matokeo tuliyopata kwenye duru ya kwanza, tunapaswa kufanya vizuri zaidi katika michezo hii ya duru ya pili," alisema Nabi
Akizungumzia utayari wa kikosi chake, Nabi amesema wataendelea kuwakosa baadhi ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbali
"Kibwana, Ninja, Yacouba, Moloko bado wanaendelea kukosekana. Kibwana na Ninja wao wamepona majeraha lakini tunaendelea kuimarisha fitnes zao"
"Tutamkosa Feisal ana kadi tatu za njano na Dickson Job ambaye anakamilisha adhabu ya kukosa michezo mitatu"
"Yassin Mustafa amerejea kikosini wakati Chico Ushindi tutaangalia utimamu wake katika mazoezi ya mwisho leo," aliongeza Nabi
Aidha Nabi amebainisha kuwa Chico Ushindi alipata majeraha ya kuchanika nyama za paja, ndio sababu amekuwa hatumiki lakini ni mchezaji mzuri ambaye atakuwa na mchango mkubwa kikosini