Katika misimu minne iliyopita Yanga ilishindwa kutwaa ubingwa wa ligi kuu, lakini uwekezaji mkubwa umefanyika msimu huu kuhakikisha Wananchi wanaumaliza ukame huo wa mataji
Ujio wa Kocha Nasreddine Nabi ni sehemu ya uwekezaji huo sambamba na usajili makini uliofanywa na GSM
Nabi amefanya mabadiliko makubwa ya kikosi msimu huu ambapo mpaka wakati huu Wananchi wakiwa wamecheza mechi 14, wanaongoza ligi pasipo kupoteza mchezo
Zipo nyakati katika misimu ambayo Yanga ilikosa ubingwa, iliongoza ligi kwa muda mrefu lakini ikapoteza nafasi ya kushinda ubingwa
Nabi amelifuatilia hilo na kubainisha kuwa msimu huu mambo yanaweza kuwa tofauti
Upana wa kikosi cha Yanga msimu huu unampa Nabi imani kuwa wakiendelea kupambana wanaweza kutimiza azma ya kushinda ubingwa
"Nafahamu hatujashinda taji la ligi kuu ndani ya misimu minne, nimefuatilia na nimebaini mapungufu ndani ya misimu hiyo ni ufinyu wa kikosi na kukosa mastaa wenye mwendelezo wa ubora kitu ambacho msimu huu tunacho"
"Nafurahi msimu huu nimeikuta timu nzuri na ina kikosi kipana ambacho akikosekana mmoja mwingine anachukua nafasi na anafanya kile kinachotakiwa kufanywa," alisema Nabi
Yanga itashuka tena uwanjani Jumatano ijayo katika mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mtibwa Sugar ambao utapigwa uwanja wa Manungu, Turiani mkoani Morogoro