Mlinzi Kibwana Shomari anaweza kurejea kikosini katika mchezo wa raundi ya tano kombe la FA dhidi ya Biashara United utakaopigwa siku ya Jumanne katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Katika mchezo huo Yanga itawakosa Shabani Djuma na Dickson Job ambao wanatumikia adhabu ya kufungiwa michezo mitatu
Djuma alifungiwa baada ya mchezo dhidi ya Polisi Tanzania na tayari amekosa michezo miwili dhidi ya Mbao Fc na Mbeya City
Job alitumika katika nafasi ya ulinzi upande wa kulia katika michezo ambayo Djuma alikosekana, nae amefungiwa mechi tatu kufuatia tukio la kumkanyaga Richardson N'gondya katika mchezo dhidi ya Mbeya City
Kama Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi ataridhishwa na utimamu wa Kibwana baada ya kuanza mazoezi, ni wazi atamtumia katika mchezo dhidi ya Biashara United
Kama sivyo atalazimika kuanza na Paulo Godfrey 'Boxer' au kiraka Deus Kaseke ambaye kwa nyakati kadhaa ametumika kama mlinzi wa kulia
Nyota wengine waliorejea kikosini baada ya kupona majeraha ni Abdallah Shaibu 'Ninja' na Yacouba Songne ambaye amekuwa nje ya uwanja wa takribani miezi mitatu
Denis Nkane na Yassin Mustafa nao wameanza mazoezi mepesi baada ya kupona majeraha