Kocha Mkuu Yanga, Nesreddine Nabi amesema amekiandaa kikosi chake kuhakikisha wanapata ushindi kwenye mchezo wa kombe la FA dhidi ya Biashara United siku ya Jumanne na pia kushinda mchezo wa Ligi Kuu ya NBC unaofuata ambao ni dhidi ya Mtibwa Sugar huko Turiani, Morogoro.
Nabi alisema mechi mbili hizo zilizoko mbele yao zina ushindani na anahitaji kupata matokeo chanya na kuendelea kujiimarisha kwenye mbio za kuchukua mataji.
Aidha Nabi amesema mchezo dhidi ya Biashara United una umuhimu wa kipekee kwa kuwa kama watapoteza basi wataondoshwa kwenye michuano ya kombe la FA lakini wakishinda watasonga mbele hatua ya robo fainali
"Hii ni mechi muhimu kwetu kwa sababu tunahitaji kutwaa ubingwa wa michuano hii, kufikia huku lazima tupambane tushinde kila mechi, lakini mechi hii ni maandalizi ya mechi yetu ijayo ya ligi, bado tunasafari ndefu, pamoja na kuongoza na ligi lakini bado hatuna uhakika wa ubingwa kwa sababu ligi ni mbio ndefu," alisema Nabi
Nabi amesisitiza kuwa ligi imekuwa na ushindani mkubwa na hakuna mwenye uhakika wa kutwaa ubingwa hadi sasa hivyo amewataka wachezaji wake kupambana katika kila mechi watakayocheza.
"Nimepata nafasi ya kuzungumza na wachezaji wangu na kuwakumbusha suala la kujituma, kucheza kwa ushirikiano, nina matarajio makubwa wachezaji wangu watazingatia hayo kwa ajili ya kufikia malengo yetu"