Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema anafurahi kuona kikosi chake kimeendelea kuimarika kwa ajili ya kuhakikisha wanatimiza malengo ya kuibuka na ushindi katika mchezo wao dhidi ya Mbeya City utakaochezwa keshokutwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam
Mbeya City wako jijini Dar es salaam kwa takribani wiki moja sasa wakijiandaa kuwakabili vinara hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao mpaka sasa hawajapoteza mchezo wowote
Nabi amesema maandalizi kuelekea mechi hiyo yanakwenda vyema na kila mchezaji anaonekana yuko tayari kuisaidia timu ipate ushindi.
Hata hivyo, Nabi alisema wachezaji wake wanatakiwa kuongeza umakini kufuatia baadhi ya matukio anayoyaona wanapokuwa katika mazoezi kwa sababu anafahamu wapinzani wao pia wamejipanga.
Kocha huyo alisema malengo yao makubwa ni kuhakikisha msimu huu wanabeba ubingwa kwa sababu hiyo kwao kila mechi wanayocheza ni sawa na fainali.
"Kikubwa ambacho tunahitaji ni pointi tatu muhimu, ili kupata pointi ni lazima tushinde mchezo wetu. Ushindani ni mkubwa na kila timu inafanya kazi kubwa kusaka pointi, kazi ni kubwa na wachezaji watahakikisha wanatekeleza kile tunachokifundisha kwenye mazoezi kwa kukipeleka uwanjani," alisema Nabi
Alisema wapinzani wao wamekuwa na kikosi imara zaidi msimu huu na wamejiandaa kukutana na ushindani mkubwa katika mechi hiyo kutokana na mabadiliko yaliyofanywa kwenye kikosi chao.
"Tunazihitaji pointi, nimeandaa kikosi changu kwa ajili ya kupata matokeo mazuri, hakuna mechi ndogo, hakuna timu ndogo, ligi hii ni ngumu, kikubwa ni kuongeza utulivu ili kujiimarisha katika mbio za ubingwa, tunapokuwa na mpira na kujipanga pale unapokuwa kwa wapinzani wetu"