Msemaji wa klabu ya Yanga Haji Manara amesema kauli za wanaosema kuwa Yanga ni kawaida yao kuongoza ligi lakini hawawezi kuchukua ubingwa ni za kujifariji tu kwani wamejipanga kutwaa ubingwa msimu
Katika mahojiano katika kipindi cha michezo cha Wasafi FM mapema leo, Manara alisema wanajivunia ubora wa kikosi na ndicho kinachowapa jeuri ya kushinda ubingwa msimu huu
"Angalia Yanga inavyocheza, passing game. Angalia wachezaji wanavyonyumbulika uwanjani, tunapiga pasi hadi milioni 300!. Tuna wachezaji bora, ukimchukua Aucho mmoja ni sawa na viungo wote wa Simba tena changanya na wale mabeki wao wazee"
"Huyo Bangala uwezo wake ni sawa na kikosi kizima cha Simba. Kocha wa makipa aliniuliza huyu anacheza Tanzania? Kila anachokifanya anafanya kwa usahihi. Hata tukifuta pointi 10 tulizowazidi sote tuwe alama 25 bado tutachukua ubingwa"
"Halafu unasikia mambo ya vichekesho na vikatuni kuwa Yanga tumezoea huwa tunaongoza lakini mwisho hatuchukui ubingwa. Haya ni maisha ya kukariri," alitamba Manara
Aidha Manara amesema baada ya kukamilisha mchakato wa mabadiliko ambao umefanyika kwa uwazi na kufuata sheria na taratibu za nchi, sasa wanaendelea na zoezi la kusajili wanachama kidigitali
"Sisi tumekamilisha mchakato wa mabadiliko, proper transformation imefanyika Yanga, hawa wengine wamefanya fanya kichupli chupli sisi tumefanya proper, bado hatujafikia pale tunapopataka, tumesajili na sasa tunasajili wanachama kidigitali"
"Mwaka huu tuna mambo mawili makubwa kama Yanga , (1) ni Ubingwa wa Ligi kuu na FA, (2) ni usajili wa wanachama kidigitali na baadaye tutakwenda kwa mashabiki haya mambo lazima yaende pamoja," alisema Manara