Wanachama wa Yanga wametakiwa kujisajili upya kupitia Kampuni za Kilinet na N-Card ili kupata idadi kamili ya wanachama hao kwa ajili ya kusaidia kutambua thamani ya nembo ya klabu yao ambayo inaelekea katika mfumo wa mabadiliko ya kiuendeshaji,
Yanga imeingia rasmi mkataba na Kilinet pamoja na N-Card katika kufanikisha mchakato huo wa usajili wa kisasa.
Kuelekea mfumo wa mabadiliko
Akizungumza jijini jana, Mkurugenzi wa Fedha wa Yanga, Haji Mfikirwa, alisema viongozi wa matawi watatakiwa kufika klabuni na kununua vitabu vya fomu pamoja na nakala ya katiba ya klabu ili kutambulika rasmi.
"Mwanachama ataenda kwenye tawi lake, atajaza fomu kwa ada ya Sh. 2,000 akiwa na picha mbili, baada ya hapo atajaza fomu na kulipa Sh. 29,000 ambapo Sh. 24,000 ni ada ya mwaka mzima na Sh. 5,000 itakuwa kwa ajili ya kodi," alisema Mfikiriwa
Alisema baada ya hapo vitabu kutoka matawini vitarudishwa klabuni na kitakachofuata ni Kilinet kuzipeleka taarifa za wahusika kwenye mtandao na kila mwanachama atapata ujumbe wa kwanza kabla ya N-Card kuthibitisha amesajiliwa rasmi na kujulishwa namba yake ya uanachama.
Naye Mkurugenzi wa Uwekezaji wa Kampuni ya GSM, Hersi Said, alisema hatua hiyo ya mwendelezo wa mchakato wao wa mabadiliko ambao walianza nayo na sasa wanaelekea hatua za mwisho.
"Kila mwanachama na shabiki anatakiwa kujiunga, na wale wote ambao wako katika makundi ya WhatsApp, hawatakuwa na ruhusa kuchangia jambo lolote la Yanga hadi watakapoonyesha au kuthibitisha wao ni wanachama waliothibitishwa," alisema Hersi