Winga wa zamani wa Yanga na timu ya Taifa Mrisho Ngasa amesema chipukizi aliyesajiliwa na Yanga Denis Nkane, ana kila sababu ya kufanikiwa akiwa na mabingwa hao wa kihistoria
Katika moja ya mahojiano yake, Nkane alimtaja Ngasa kama mchezaji anayemkubali zaidi na alikuwa akimfuatilia kwenye mechi za Yanga na timu nyingine alizokuwa akicheza
"Mimi namkubali sana Ngasa, nimefuatilia tangu mwanzo wakati anacheza Yanga, akaondoka kujiunga na Simba, Azam na hata aliporudi Yanga kwa mara ya tatu," alisema Nkane
Aina ya uchezaji wa Nkane wengi wamemfananisha na Ngasa, wakimtabiria kufanya mambo makubwa siku za usoni
Ngasa amesema anamuona Nkane akifanikiwa Yanga, muhimu awe na nidhamu na kujituma katika kutimiza majukumu yake
"Mimi namtakia kila la kheri, siri ya mafanikio ni kujituma na nidhamu, naamini atafanikiwa, wadau tunapaswa kumuunga mkono," alisema Ngasa
Aidha mkongwe huyo alisema kuwa angependa kuona Nkane akikabidhiwa jezi namba 16 ambayo yeye amekuwa akiitumia