Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema kuwa mlinzi wa kulia wa timu hiyo Djuma Shabani alipata majeraha kwenye mchezo uliopita dhidi ya Biashara United ambao ulimalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-1
Akizungumza katika Mkutano na Wanahabari kuelekea mchezo dhidi ya Dodoma Jiji ambao utapigwa kesho Ijumaa, katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Kaze amesema Djuma hajafanya mazoezi na timu tangu alipopata majeraha na watamfanyia tathmini baada ya mazoezi ya mwisho leo
Hata hivyo Kaze amesema wachezaji wengine wote ukiondoa Kibwan Shomari, Yusufu Athumani na Yacouba Songne, wako tayari
Katika hatua nyingine, Kaze amethibitisha kuwa Yanga imekusudia kusajili mchezaji wa kigeni ili kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji
Kaze amesema wanaendelea kuwafanyia tathmini wachezaji kadhaa kwani wanahitaji kusajili mchezaji ambaye ana uwezo zaidi ya hawa waliopo
"Ni kweli tunatafuta kusajili mchezaji wa kigeni kwa ajili ya nafasi ya ushambuliaji. Lakini ni lazima mchezaji huyo awe bora kuliko hawa tulionao. Kwani tunahitaji mchezaji ambaye ataongeza kitu katika timu yetu," alisema Kaze