Mfumo ambao kocha Nasreddine Nabi alitumia kwenye mchezo dhidi ya Simba uliopigwa mwishoni mwa wiki na kumalizika kwa suluhu ya bila kufungana ni kama uliwarahisishia kazi walinzi wa Simba Joash Onyango na Hennock Inonga kuweza kumdhibiti mshambuliaji hatari wa Yanga, Fiston Mayele
Katika mchezo huo Nabi alitumia mfumo wake wa 4-2-3-1 lakini akichukua tahadhari kwa kumrudisha Fei Toto chini zaidi
Fei Toto alikuwa akirudi katikati kusaidiana na Yannick Bangala na Khalid Aucho ambapo Yanga ilifanikiwa kutawala eneo la kiungo lakini ikakosa idadi nzuri ya watu wakati wa kushambulia
Mayele alikuwa peke yake mbele muda mwingi wa mchezo na hivyo ikawa rahisi kwa walinzi hao kuonekana wako bora mbele yake
"Nimezoea kucheza mbele na Fei Toto ila kwenye dabi alikuwa mbali, ndio maana Onyango na Inonga ilikuwa rahisi kukutana na mimi mbele ama walikuwa wananiona kirahisi," alisema Mayele baada ya mchezo huo ambao matokeo yake yalishangiliwa sana na mashabiki wa Simba
Aidha kukosekana kwa mshambuliaji Yacouba Songne pia kuliwapa nafasi walinzi hao kuwa huru kwani pamoja na Saido Ntibazonkiza kun'gara hasa kwenye kipindi cha pili, katika kipindi cha kwanza alikuwa akicheza chini sana
Yacouba ataendelea kukosekana katika kikosi cha Yanga pengine mpaka mwishoni mwa msimu baada ya kufanyiwa upasuaji wa goti mwezi uliopita
Yanga inatarajiwa kusajili mshambuliaji mwingine katika dirisha dogo la usajili litakalofunguliwa Jumatano Disemba 15