Muda mchache ujao, Yanga itakuwa uwanjani pale Sokoine kuikabili Mbeya Kwanza katika mchezo wa ligi kuu ya NBC
Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi jana aliweka bayana kuwa kikosi chake leo kitakuwa na mabadiliko kutokana na sababu mbalimbali
Wapo wachezaji ambao wanakosekana kutokana na kuwa majeruhi (Jesus Moloko na Yacouba Songne), Yannick Bangala yeye anatumikia adhabu ya kadi tatu za njano
Kwa mara ya kwanza msimu huu Moloko atakosekana kwenye timu inayoanza, Deus Kaseka ambaye mara nyingi ametumika kama mbadala wake huenda akaanza
Hakuna shaka Mukoko Tonombe leo atakuwa tegemeo eneo la kiungo na pengine anaweza kuanza na pacha wake wa msimu uliopita, Zawadi Mauya
Kuna uwezekano mdogo Khalid Aucho akacheza kutokana na mazingira ya mchezo huo huku yeye akitokea kwenye majeraha na pia akiwa na kadi mbili za njano
Farid Mussa amekuwa akitumika kama mbadala wa Yacouba lakini pia mkongwe Saido Ntibazonkiza yupo tayari kuwapa raha mashabiki wa Yanga mkoani Mbeya kama Nabi atampa nafasi ya kuanza
Lakini pia wapo kina Dickson Ambundo na Mapinduzi Balama ambao wamerejea kikosini baada ya kupona majeraha
Safu ya ulinzi haitarajiwi kuwa na mabadiliko kama ilivyo kwa safu ya ushambuliaji ambayo Nabi anamtumia Fiston Mayele kama mshambuliaji kiongozi na Feisal Salum 'Fei Toto' akicheza namba 10
Ni mchezo ambao Yanga inahitaji kushinda ili kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi