Baada ya kulazimishwa sare ya bao 1-1 dhidi ya Namungo Fc katika mchezo uliopita, kikosi cha Yanga kimepania kuondoka na alama zote tatu katika mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza ambao utapigwa Jumanne kwenye uwanja wa Sokoine
Yanga iliwasili Mbeya mapema jana na jioni kupata nafasi ya kufanya mazoezi yake ya kwanza mkoani humo
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema walichokifuata mkoani Mbeya ni alama tatu ili kuendelea kujikita kileleni mwa msimamo wa ligi kuu ya NBC
Amesema matokeo waliyopata kwenye mchezo uliopita dhidi ya Namungo Fc wameyasahau ila wamejipanga kuhakikisha matokeo hayo hayajirudii mkoani Mbeya
"Mchezo uliopita tulitoka sare na Namungo, ndugu zetu Mbeya Kwanza watatusamehe kwani hatuhitaji matokeo mengine zaidi ya ushindi"
"Tunafahamu kila mchezo wa ligi ni mgumu, hivyo haitakuwa rahisi kupata ushindi lakini tumejiandaa vya kutosha kuhakikisha tunatimiza malengo yetu," alisema Bumbuli
Yanga ilitua mkoani Mbeya ikiwa na kikosi chake kamili, Yannick Bangala akikosekana akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano wakati Yacouba Songne ni majeruhi