Asikwambie mtu! Hii Yanga wanaiogopa sana. Si wameuona mziki wa Wananchi katika zile mechi nne za mwanzo baada ya Kocha Nasreddine Nabi kupata kikosi chake cha kwanza!
Iko hivi; Jumanne Wananchi watakuwa mkoani Mbeya kwenye mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mbeya Kwanza ambao utapigwa uwanja wa Sokoine
Baada ya mchezo huo, Wananchi watarejea jijini Dar es salaam kujiandaa na mchezo dhidi ya Simba ambao utapigwa Disemba 11
Kiungo Yannick Bangala hatakuwa sehemu ya mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza akitumikia adhabu ya kadi tatu za njano hivyo kwa sasa anaandaliwa kwa ajili ya mchezo dhidi ya Simba
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema wameshtukia mpango wa kuwakwamisha baadhi ya nyota wao kuelekea mchezo dhidi ya Simba
Bumbuli amesema watakuwa makini zaidi kwenye mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza ambapo huenda wakalazimika kuwapumzisha baadhi ya wachezaji ili kuhakikisha wanakuwa sehemu ya mchezo dhidi ya Simba
"Tutakuwa makini zaidi kwenye mechi yetu dhidi ya Mbeya Kwanza, tunajua mipango iliyopo, tutafanya hivi kujiweka katika nafasi salama kwa sababu tunahofia kupata kadi za njano na kupelekea baadhi ya nyota kuukosa mchezo dhidi ya Simba hapo Desemba 11, hili tumeshalifanyia kazi"
"Tumebaini janja janja za wapinzani wetu kuwatafutia kadi za njano wachezaji wetu nyota, au kufanyiwa rafu za makusudi akiwamo, Khalid Aucho na wengine ili kushindwa kucheza mechi ijayo dhidi ya Simba,"
"Tumegundua na tunatarajia mechi yetu dhidi ya Mbeya Kwanza itakuwa na mabadiliko katika kikosi, baadhi ya nyota watapumzishwa kwa ajili ya kujiandaa na pambano letu dhidi ya Simba, tunawahakikishia mashabiki wetu tutarejea na pointi tatu kutoka kwa Mbeya Kwanza halafu Desemba 11, tabu iko pale pale dhidi ya Simba," alisema Bumbuii
Aucho ana kadi mbili za njano, kama atatumika kwenye mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza na akaonyeshwa kadi ya njano basi atakosa mchezo dhidi ya Simba
Kwa fitna za soka letu, ni wazi kama Aucho atacheza mchezo dhidi ya Mbeya Kwanza anaweza kutafutiwa kadi ya njano ili kuikosa Simba
Kwa sababu ndiye mchezaji wanayemhofia zaidi kwenye kikosi cha Yanga wakiamini yeye ndiye 'engine' ya timu