Mchezo wa kwanza kwenye ligi utakao wakutanisha watani wa jadi Yanga na Simba, utapigwa Disemba 11 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa
Simba watakuwa wenyeji wa mchezo huo wa nne kuzikutanisha timu hizo mwaka huu
Shamra shamra kuelekea mchezo huo zimeanza mapemaa, propaganda zikiendelea kushika kasi kwenye mitandao ya kijamii
Mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Mkutano Mkuu wa Wanachama wa Simba, ajenda kubwa ilikuwa mchezo huo uongozi wa Simba ukiwaahidi Wanachama wao kuwa watashinda
Kwa misimu ya karibuni, Yanga imedhihirisha ubabe wake dhidi ya watani Simba ambapo katika misimu miwili iliyopita, Simba haijaweza kuondoka na ushindi mbele ya Yanga
Afisa Mhamasishaji wa Yanga Haji Manara amesema kwao mchezo dhidi ya Simba ni wa kawaida kama ilivyo michezo mingine na wataendeleza umwamba wao
Manara amesema timu waliyoifunga kuliko zote ni Simba na timu waliyoifunga mabao mengi kuliko zote ni Simba hivyo kipigo kitawahusu tena Disemba 11
Timu hizo zilikutana kwenye mchezo wa Ngao ya Jamii na Yanga kuondoka na ushindi wa bao 1-0
Yanga imeimarika maradufu ukilinganisha na iliyotwaa Ngao ya Jamii Septemba 25 ikiongoza ligi kuu baada ya kushinda michezo mitano na kutoka sare mchezo mmoja, alama 16
Ubora wa kikosi unawapa Wananchi jeuri ya kutamba kuwa wataibuka na ushindi Disemba 11