Kocha Msaidizi wa Yanga Cedric Kaze amesema baada ya mchezo dhidi ya Namungo Fc uliomalizika kwa matokeo ya sare ya bao 1-1, wanajipanga kwa ajili ya mchezo unaofuata dhidi ya Mbeya Kwanza ambao utapigwa Novemba 30 katika uwanja wa Sokoine
Yanga ilirejea jijini Dar es salaam jana wakitokea mkoani Lindi ambako walipoteza alama mbili za kwanza msimu huu
Akizungumzia mchezo dhidi ya Namungo Fc, Kaze alisema pamoja na changamoto za uwanja, vijana hawakuwa katika ubora wao
"Pamoja na tatizo la uwanja, nafikiri pia hatukuwa bora kwenye mchezo kwa ujumla. Tulijua kuwa watacheza mipira mirefu, lakini tukawaacha wakaipiga, wakaikamata, hata wakati mipira inaanguka kati wakati inaokolewa, bado tukawaacha wakaimiliki, ni vitu vingi havikwenda vizuri," alisema Kaze
Kaze amesema kuwa wanafanyia kazi mapungufu yaliyojitokeza na muhimu zaidi ni kuhakikisha wanakuwa bora katika michezo itakayochezwa kwenye viwanja visivyo bora
"Ili tuweze kushinda ubingwa, inabidi wachezaji wetu waweze kucheza kwenye viwanja vya aina zote, vizuri na vibovu, hivyo inabidi sasa tujielekeze kuwafundisha jinsi ya kucheza kwenye aina mbalimbali za viwanja, lakini pamoja na hayo tunashukuru kwa kupata pointi moja, tunakwenda kujipanga"