Tanzania ina dakika 180 muhimu kuandika historia kwa kuvuka hatua ya mtoano na pengine kukata tiketi ya kushiriki michuano ya kombe la Dunia itakayofanyia nchini Qatar mwakani
Hesabu ya dakika hizo inaanza leo pale uwanja wa Benjamin Mkapa Tanzania ikiwa mwenyeji wa DR Congo katika mchezo ambao alama tatu kwa Tanzania zitakuwa na thamani kubwa
Tanzania ni vinara kundi J wakiwa na alama saba, kama ilivyo kwa Benin lakini Tanzania ikiongoza kwa faida ya mabao ya kufunga
DR Congo wana alama tano wakiwa nafasi ya tatu, kimahesabu nao wataweka hai matumaini ya kusonga mbele kama watapata ushindi lakini wataondoshwa mashindanoni kama watafungwa leo
Hivyo ni mchezo ambao utakuwa na upinzani mkali, utakuwa kipimo sahihi kwa Tanzania kudhihirisha nia na dhamira ya kucheza kombe la Dunia mwakani
Tanzania iliingia kambini mwishoni mwa wiki iliyopita kocha Kim Poulsen akiahidi ushindi katika mchezo huo
Watanzania wameaswa kujitokeza kwa wingi uwanja wa Benjamin Mkapa kuiunga mkono Stars, CAF ikiruhusu mashabiki 30,000 kuingia uwanjani kushuhudia mchezo huo
Mchezo utapigwa kuanzia saa kumi kamili alasiri
Kila la kheri Tanzania, kila la kheri timu yetu ya Taifa