Msemaji wa Yanga Haji Manara amesema mchezo dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa Jumamosi, Oktoba 30 kwenye uwanja wa Benjamin Mkapa, utaambatana na burudani mbalimbali
Manara amesema kama klabu wamekuja na utaratibu wa kuzifanya mechi zote wanazocheza nyumbani kuwa sehemu ya burudani kwa mashabiki wao
Jumamosi kabla ya mchezo kutakuwa na burudani za utangulizi kutoka kwa wasanii mbalimbali, utaratibu ambao wataufanya kwa michezo yote wanayocheza nyumbani
"Tunataka mechi zetu iwe sehemu ya burudani, mashabiki wanapotoka nyumbani kuja uwanjani, watakuwa wakipata burudani mbalimbli kabla ya mchezo. Barani Ulaya jambo hili wanafanya nasi tumeona si vibaya kulianzisha kwa kuanzia Jumamosi kwenye mchezo dhidi ya Azam," alisema Manara
"Kutakuwa na burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali ambao majina yao tutayatangaza, lengo ni kuifanya siku hiyo shabiki aweze kutoka kwake na familia yake kufuata burudani kama tunavyofanya kwenye wiki ya Mwananchi"
Akizungumzia mchezo dhidi ya Azam Fc, Manara amesema mshindani wao halisi katika mbio za ubingwa msimu huu ni Azam Fc hivyo wanawaheshimu
Lakini amesema Yanga imejipanga kushinda ubingwa hivyo watahakikisha wanaondoka na alama zote tatu