Kiungo wa Yanga Mukoko Tonombe amesema mashabiki wana kila sababu ya kuwa na imani na timu yao msimu huu kwani wanayo nafasi ya kushinda ubingwa
Wananchi wameanza msimu kibabe kwa kushinda michezo yote mitatu ya mwanzo na hivyo kukaa kileleni katika msimamo wa ligi
Mukoko ambaye juzi alitajwa kwenye kikosi bora cha msimu uliopita, amesema Yanga sasa imeiva huku akitoa shukrani kwa wadhamini GSM pamoja na mashabiki kwa kuendelea kuwaunga mkono
Nahodha huyo msaidizi wa Yanga bado hajapata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza baada ya kukosa mchezo uliopita dhidi ya KMC
Alikosa mechi tatu za mwanzo, Ngao ya Jamii na mechi mbili za ligi akitumikia adhabu ya kadi nyekundu aliyopewa kwenye mchezo wa fainali kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Simba msimu uliopita
Hata hivyo Mcongomani huyo amesema anafurahia kazi inayofanywa na wachezaji wenzake na kuwa atajipanga ili kuweza kupata nafasi ya kucheza
Mukoko amesema anatambua ni vigumu kwa kocha Nesreddine Nabi kuanza kubadilisha sura ya kikosi kutokana na ubora ambao unaendelea kuonekana
"Najua sababu. Wala sina tatizo kubwa katika hilo, mnakumbuka sikuwa naruhusiwa kucheza baada ya kusimamishwa, pia naona ubora wa timu kwa sasa upo juu, hii ni sababu na lazima nipambane," alisema Mukoko
"Namuelewa pia kocha (Nabi) ni vigumu kwake kubadilisha kikosi kwa sasa kwani timu inashinda, timu ikishinda sio tu wale wanaocheza sote tunafurahia, maana ndio malengo yetu na ndio sababu tuko hapa"
"Wenzangu (Aucho na Bangala) nao wanacheza vizuri na wanaonekana kutulia na kutuliza timu, kwanza lazima uwapongeze kisha uwe na akili ya kujua utapataje nafasi mbele yao, hiki ndicho ninachokifanya sasa"