Baada ya mapumziko ya siku chache, Wananchi wamerejea kambini kujiandaa na mchezo wa ligi kuu dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa Oktoba 30 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Kocha Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi, amesema kikosi chake kimeendelea na programu tofauti kwa sababu kila idara inahitaji kupata mbinu ili kufikia malengo.
Kocha huyo mwenye uraia pacha wa Tunisia na Ubelgiji, amesema anahitaji kuona kila mchezaji anatekeleza vyema majukumu yake katika mchezo huo ambao endapo watashinda, wataendelea kuongoza kwenye msimamo wa ligi
"Tunaijua Azam FC, ni timu bora na ina wachezaji wenye viwango vizuri, wameshinda mechi yao iliyopita, ni wazi wanahitaji kuendelea na ari hiyo, sisi pia tunataka kushinda ili kujiimarisha, tutapambana tu," alisema Nabi.
Aliongeza wanajiandaa kukutana na timu yenye kutumia nguvu kwa sababu watakuwa wametoka kwenye mchezo wa pili wa kimataifa ambao utawasaidia kuwajenga nyota wake.
Huu utakuwa mchezo wa pili kwa Kocha Nabi dhidi ya Azam Fc akipotezza mchezo wa kwanza msimu uliopita kwa kufungwa bao 1-0
Ilikuwa April 23, siku mbili tangu Nabi akabidhiwe mikoba ya kukinoa kikosi cha Yanga. Wakati ule alikuwa bado hajaanza kuingiza mbinu zake kwenye timu
Lakini sasa pamoja na usajili makini uliofanyika, ni wazi Azam Fc watarajie kukutana na Yanga nyingine kabisa