Kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi amesema kila mchezaji katika kikosi chake anapaswa kuipigania nafasi yake ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza
Aidha Nabi amesema hana tatizo na mchezaji yeyote akiwemo mkongwe Saido Ntibazonkiza, uamuzi wa kumtumia au la utategemea na utayari na utimamu wake
Kumekuwa na maswali mengi kuhusu Saido ambaye ameachwa nje katika michezo yote mitatu ya mwanzo ligi kuu msimu huu
"Sina tatizo na mchezaji yeyote, Saido ni sehemu ya hii timu na tuko naye ingawa hakusafiri nasi Kagera na Ruvuma. Kazi aliyonayo ni kupigania nafasi yake kwenye timu"
"Nikiona anaimarika kama ninavyotaka nitampa nafasi, sina tatizo na mchezaji ambaye naona anaweza kusaidia hii timu, tunahitaji mafanikio na kazi hiyo itafanywa na sisi makocha na wachezaji," alisema Nabi
Katika kikosi cha Yanga msimu huu kina ushindani mkali wa nafasi kutokana na ubora wa wachezaji waliosajiliwa katika dirisha lililopita
Katika mchezo dhidi ya KMC, Saido na Mukoko Tonombe hawakuwa sehemu ya kikosi kutokana na sheria ya wachezaji nane wa kigeni kutumika katika mchezo mmoja
Sheria hii huenda ikaongeza ushindani miongoni mwa wachezaji wa kigeni, Yanga ikiwa imesajili wachezaji 10 lakini wanaoruhusiwa kutumika katika mchezo mmoja ni nane tu