Mlinzi Dickson Job ni miongoni mwa wachezaji wanaofanya vizuri sana katika kikosi cha Yanga
Job amekuwa mchezaji tegemeo kwenye safu ya ulinzi akishirikiana vyema na nahodha bakari Nondo Mwamnyeto
Katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar Job alianza kwenye safu ya ulinzi na Yannick Bangala baada ya Mwamnyeto kupata majeraha katika kidole
Wiki iliyopita Yanga ilimtambulisha Cedric Kaze kuwa Kocha Msaidizi wa Yanga ikiwa ni takribani miezi sita tangu alipoondolewa kwenye majukumu ya kocha mkuu
Kaze ndiye aliyependekeza usajili wa Job wakati akiwa kocha mkuu
Wakati anapendekeza Job asajiliwe kutoka Mtibwa Sugar, Yanga ilikuwa na walinzi tegemeo wakiongozwa na aliyekuwa nahodha Lamine Moro, Mwamnyeto, Abdallah Shaibu na Said Juma Makapu
Alipoulizwa kwa nini anamtaka Job licha ya safu yake ya ulinzi kuwa imekamilika, Kaze alisema alihitaji mlinzi ambaye anaweza kumtumia katika kujenga mashambulizi kutokea nyuma
Kwa hakika ni kazi ambayo Job amekuwa akiifanya kwa umahiri sana katika kikosi cha Yanga
Wakati ule Kaze hakuweza kumtumia Job kwenye kikosi chake kwa sababu alikuwa majeruhi
Lakini kocha huyo raia wa Burundi sasa anamshuhudia Job akifanya kile alichohitaji aje akifanye