Kikosi cha Yanga leo kinakamilisha maandalizi ya mwisho kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba ambao utapigwa kesho Jumamosi katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Kwa takribani siku nne, Yanga wamejifua kisawasawa Avic Town kujiandaa na mchezo huo ambao wanahitaji kushinda
Nahodha wa Yanga Bakari Nondo Mwamnyeto amesema baada kutolewa katika michuano ya ligi ya mabingwa, wamepania kurejea katika mashindano ya ndani kwa nguvu
Mwamnyeto amesema kurejea kikosini kwa wachezaji waliokuwa majeruhi na wengine waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya ITC, kumewaongezea nguvu kuelekea mchezo huo
"Tunashukuru tuko imara, majeruhi wamerudi na wengine hatukuwa nao awali katika ligi ya mabingwa, ni jambo jema kwetu, morali ya wachezaji wote iko juu," alisema Mwamnyeto
Mchezo dhidi ya Simba kesho utakuwa wa kisasi kwa Yanga baada ya kupoteza mchezo wa fainali kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) Juali 25 mkoani Kigoma