Msemaji wa klabu ya Yanga Haji Manara amesema bado hawajapokea majibu ya maombi waliyopeleka kwa Shirikisho la Soka Barani Afrika (CAF) kuhusu idadi ya mashabiki ambao wataruhusiwa kuingia uwanjani kushuhudia mchezo wa ligi ya mabingwa kati ya Yanga dhidi ya Rivers United
Manara amesema mpaka itakapofika mchana wa leo, viongozi wa Yanga na TFF watakaa ili kuamua nini kifanyike
"Tuliwaandikia barua CAF kupitia TFF kuwauliza idadi ya mashabiki ambao tutaruhusiwa kuwapeleka uwanjani mchezo dhidi ya Rivers United lakini mpaka sasa hawajatujibu"
"Ni jambo ambalo limetushangaza kwani imekuwa kawaida yao kutoa maelekezo hayo mapema, kama itafikia mchana wa leo na hakutakuwa na taarifa kutoka CAF sisi viongozi wa Yanga kwa kuwashirikisha TFF tutakaa ili tupate mwafaka," alisema Manara
Manara pia amesema bado hawajapokea majibu ya barua waliyoandika FIFA wakiomba ruhusa ya kuwatumia wachezaji Shabani Djuma, Khalid Aucho na Fiston Mayele ambao ITC zao ziliwasili siku moja baada ya dirisha la usajili wa michuano ya CAF kufungwa
"Pia hatujapokea majibu ya FIFA kuhusu wachezaji wetu lakini tunayo imani FIFA watatujibu hata kama watachelewa"