Wakati ikisubiriwa taarifa ya CAF kuhusu idadi ya mashabiki ambao wataruhusiwa kushuhudia mchezo wa hatua ya awali ligi ya mabingwa kati ya Yanga dhidi ya Rivers United ambao utapigwa Jumapili Septemba 12 katika uwanja wa Benjamin Mkapa, Msemaji wa klabu ya Yanga Haji Manara amesema watakaopata fursa ya kuingia dimba la Mkapa wanapaswa kushangilia muda wote ili kuwapa presha wapinzani wao
Manara amesema bado hawajapokea taarifa CAF kuhusu idadi ya mashabiki, taarifa zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuhusu mchezo huo kuchezwa bila ya mashabiki hazina ukweli
"Bado hakuna taarifa rasmi kutoka CAF, taarifa zinazosambazwa kuwa mchezo utachezwa bila ya mashabiki hazina ukweli wowote. Muhimu, kwa idadi yoyote ya mashabiki ambao tunaweza kuruhusiwa, watapaswa kushangilia kwa muda wote wa mchezo," alisema Manara
Akizungumzia maandalizi ya Yanga kuelekea mchezo huo, Manara amesema mpaka sasa kila kitu kiko sawa, wamepania kumaliza mchezo huo hapa nyumbani
"Kama klabu tumejipanga kwenda kupata matokeo mazuri ambayo yatatusaidia kwenye mchezo wa marudiano. Tunamuamini kocha wetu (Nabi) kwani ana uwezo mkubwa sana wa kuwasoma wapinzani," alisema Manara katika mahojiano katika kipindi cha michezo EFM