Ukipita kwenye mitandao ya kijamii mjadala ni kukosekana kwa baadhi ya wachezaji ambao ITC zao hazikufika kwa wakati
Kuna watu wanatumia nguvu kubwa kuwakatisha tamaa mashabiki wa Yanga kwa kuwaaminisha kuwa kukosekana kwa wachezaji hao kunaweza kuigharimu Yanga kwenye mchezo wa Jumapili dhidi ya Rivers United
Ifahamike kuwa uongozi wa Yanga ulifanya kila jitihada kuziomba ITC za wachezaji hao kwa wakati lakini yaliyotokea yalikuwa nje ya uwezo wao
Ni kweli, Wanayanga walipenda kuwaona Shabani Djuma, Fiston Mayele na Khalid Aucho katika mchezo dhidi ya Rivers United kwa kuwa wanatambua uwezo wao na wamesajiliwa ili kukiongezea nguvu kikosi kwenye michuano hiyo mikubwa, lakini kukosekana kwao haiwezi kuwa sababu ya Yanga kukosa matokeo
Yanga ina kikosi imara ambacho kinaweza kuivusha timu hatua ya makundi, wachezaji waliosajiliwa kwa ajili ya michuano ya ligi ya mabingwa wako 28, watakaokosekana ni watatu tu
Habari njema ni kuwa nafasi za wachezaji hao tayari zina watu ambao hata wakiamshwa saa sita usiku wako tayari kuipambania Yanga
Kibwana Shamari amekuwa mchezaji bora katika kikosi cha Yanga, kukosekana kwa Djuma kunampa nafasi kutumika katika eneo analolimudu zaidi
Mshambuliaji Heritier Makambo amerejea na hana changamoto ya ITC hivyo kukosekana kwa Mayele haliwezi kuwa pengo kwa Yanga
Aucho ni moja ya sajili bora zilizofanywa katika dirisha la usajili lililopita, hata hivyo amefanya mazoezi na timu siku moja tu nchini Morocco kabla ya kurejea Uganda kwa ajili ya majukumu ya timu ya Taifa
Kocha Nasreddine Nabi amefanya maandalizi ya kikosi chake pasipo kumtegemea mchezaji huyo ambaye atawasili nchini kesho kuungana na wenzake
Hata kama asingekuwa na changamoto pengine Nabi asingemtumia kwani atakuwa amefanya mazoezi na timu kwa siku tatu tu
Nawakumbusha tu, Julai 03 Yanga iliichapa Simba bao 1-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa hapo kwa Mkapa
Ukiwaondoa mlinda lango Farouk Shikhalo na winga Tuisila Kisinda, wachezaji wengine wote wa kikosi kile bado wapo
Nabi anaweza kutumia kikosi kilekile kwa kuwaongeza mlinda lango Djigui Diarra nafasi ya Shikhalo, winga yupo Jesus Moloko nafasi ya Kisinda huku Herietier Makambo akiongezeka katika eneo la ushambuliaji kusaidiana na Yacouba Songne
Safu ya ulinzi au kiungo cha ukabaji anaweza kumuongeza Yannick Bangala Litombo kuunda kikosi ambacho kinaweza kumpiga yeyote hapo kwa Mkapa
Kiufupi, Yanga iko imara bila ya wachezaji hao na itakuwa imara zaidi pale watakapoanza kutumika