Mkurugenzi wa Sheria klabu ya Yanga Simon Patrick ametoa ufafanuzi ufuatao kuhusu uteuzi wa Kaimu Mtendaji Mkuu wa Yanga Senzo Mazingisa, uteuzi ambao umefanyika hivi karibuni
Wapo baadhi ya wanachama na mashabiki waliohoji uhalali wa uteuzi wa Senzo wakiamini nafasi hiyo ilipaswa kushikiliwa na Mtanzania
Hata hivyo kulingana na Katiba ya Yanga iliyopitishwa na Wanachama Juni 27, 2021, uteuzi huo hauna shaka; Simon ametoa ufafanuzi zaidi wa kisheria
"Ofisi ya Mtendaji mkuu imeundwa na ibara ya 37(3) ya Katiba Mpya ya Yanga ya Mwaka 2021 kama sehemu ya menejimenti ya Klabu
Ibara ya 37 imeunda Timu ya Menejimenti ya Yanga kuwa na idara zifuatazo; Ofisi ya Mtendaji Mkuu, ambapo chini yake kuna Idara ya Katiba na Sheria, Idara ya Habari (PR), Idara ya Fedha, Idara ya Uwekezaji na Masoko, Idara ya Michezo, na Idara ya Wanachama na Mashabiki
Pia ibara ya 37(4) ya Katiba imeipa mamlaka Kamati ya Utendaji kuunda idara nyingine yeyote pale itakapoona inafaa na kuna uhitaji.
Idara zote hizi zinakuwa chini ya ofisi ya Mtendaji Mkuu. - Pale itakapofunguliwa Kampuni kwa ajili ya wawekezaji kuja kuwekeza, idara hizi zote zitafanya kazi chini ya hiyo kampuni kwa makubaliano maalum kama ilivyoainishwa chini ya ibara ya 37(6), hii inamaana kampuni ikishafunguliwa itazikuta hizi idara.
Kwa maana hiyo, uteuzi wa Mr. Senzo kuwa Mtendaji Mkuu wa mpito unamaana kwamba anakuwa Mkuu wa hizo idara zote katika kipindi chote cha mabadiliko mpaka pale kampuni itakavyofunguliwa na kuwa na bodi yake ya Wakurugenzi, na bodi ya wakurugenzi chini ya kampuni itakayofunguliwa itakuwa na maamuzi ya kumteua Mtendaji Mkuu watakayeona anafaa, pia wanaweza kuamua waendelee na Senzo au mtu mwingine.
Hii ndio sababu kubwa ya Kamati ya Utendaji kuamua kumteua Mr. Senzo Mazingiza kuwa Mtendaji Mkuu wa Mpito (Interim CEO)"
NB: Katiba ninayoizungumzia hapa ni ile iliyopitishwa na Wanachama wa Yanga kwenye mkutano mkuu wa tarehe 27 Juni 2021.