Wanachama na viongozi wa Yanga Tanzania wametakiwa kuendeleza Umoja na Mshikamano kwa maslahi ya timu yao
Wito huo umetolewa na Makamu wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdallah katika hafla ya uzinduzi wa wiki ya Mwananchi iliyofanyika katika ukumbi wa mkutano Kariakoo mjini Unguja hapo jana
Hemed ambae aliwakilishwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Idara Maalumu za SMZ Masoud Ali, amesema umoja huo utakuwa na maana sana kwa ajili ya maendeleo na mafanikio kwa klabu yao
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Habari na Hamasa wa klabu ya Yanga Suma Mwaitenda alisema katika siku hiyo ya wananchi ambayo itaadhimishwa Agosti 29 mwaka huu, kutakuwa na shughuli mbali mbali ikiwemo burudani na soka huku akiwasisitiza Wanayanga kufanya mambo mazuri kwa Jamii.
Mapema Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolwa ambae aliwakilishwa na Mjumbe wa kamati tendaji ya Yanga Saad Mohammed Kimji, aliishukuru Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa ushirikiano wao waliowapa tokea walipofika visiwani Zanzibar
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo Fatma Hamad Rajab amesema Wizara inaipongeza Yanga kwa kuja kufanya Uzinduzi wa Wiki ya Mwanachi Visiwani Zanzibar.
Wiki hiyo ya Mwananchi ilianza mapema saa 3 asubuhi kwa Maandamano yaliyoanzia Kariakoo na Kwenda Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui kwaajili ya kuzuru kwenye Kaburi la Marehemu Abeid Aman Karume ambae ni muasisi wa Yanga
Wiki hiyo ya Mwananchi itahitimishwa Agost 29, 2021 Uwanja wa Mkapa Dar es salam