Kumekuwa na taarifa zinaenea kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuondoka kwa wataalamu watatu wa benchi la ufundi kocha msaidizi, Sighr Hamad, mtaalamu wa mazoezi ya viungo Jawad Sabri na daktari Msauzi wa viungo Fareed Cassem
Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Injinia Hersi Said amethibitisha kuondoka kwa wataalamu hao ambao wamepata changamoto mpya mahali pengine
Hata hivyo akadokeza walikuwa katika mchakato wa kuliboresha benchi la ufundi kulingana na mapendekezo ya kocha Nasreddine Nabi
Kocha Nabi mwenyewe alithibitisha kuwepo kwa mabadiliko katika benchi lake ambapo amesema kocha msaidizi anatarajiwa kuingia kambini wakati wowote akitokea klabu ya Esperance
"Kuna mtu nimemleta kutoka Tunisia toka klabu ya Esperance ni kocha mzuri sana atakuja hapa haraka wakati wowote kuanzia leo (jana mchana) kuja kuanza kazi, huyu ni kocha mzuri sana nampongeza Gharib (GSM) kwa kusimamia vyema kumleta," Nabi alinukuliwa na Mwanaspoti
Nabi alisema mtu wa pili ambaye ni mtaalamu wa mazoezi ya viungo naye ataungana na timu hiyo haraka wakati wowote kuanzia leo kuja kuendeleza pale alipoishia Jawad ambaye tayari alishaanza kukubalika kwa mazoezi yake kikosini
Mtaalamu wa tatu kati ya hao ni daktari wa viungo tayari ameshatua kambini akitambulika kwa jina la Youssef Ammar ambaye tayari ameshaanza kazi rasmi ndani ya timu hiyo akichukua nafasi ya Cassem