Ukiacha mahusiano mazuri ambayo Yanga wametengeneza na wachezaji kutoka DR Congo, uwepo wa wachezaji wengi kutoka nchi hiyo katika kikosi msimu ujao utakuwa na manufaa
Nyota sita wa DR Congo watakaoitumikia Yanga msimu ujao ni Shabani Djuma, Yannick Bangala, Mukoko Tomombe, Jesus Moloko, Heritier Makambo na Fiston Mayele
Ukimuondoa Makambo, wachezaji watano waliosajiliwa wamecheza pamoja klabu ya AS Vita
Ni wachezaji ambao wanafahamiana vizuri, hivyo watampa kazi rahisi kocha Nasreddine Nabi kuwaunganisha na wenzao
Mukoko, Djuma, Mayele na Bangala pia wamecheza pamoja katika timu ya Taifa. Makambo amecheza Horoya Ac ambayo msimu uliopita ilitinga robo fainali ya ligi ya mabingwa. Yeye sio mgeni Yanga, alicheza hapa misimu miwili iliyopita na akafunga mabao 22 katika mashindano yote
Pia nyota hawa wanazungumza lugha ya Kifaransa na kiswahili japo kidogo, hawatakuwa na changamoto katika kuwasiliana na wachezaji wa Kitanzania
Kiungo Khalid Aucho, ni mchezaji wa daraja la juu ambaye hatahitaji muda mrefu kuzoeana na wenzake. Yeye anazungumza kiingereza na kiswahili kidogo pia
Dickson Ambundo, Bryson David wamefanya vizuri kwenye ligi msimu uliomalizika. Msimu mmoja nyuma, Ambundo alikuwa nchini Kenya akiitumikia klabu ya Gor Mahia
Ni mchezaji aliyezoea haraka mazingira, juzi tu Yanga ilimtumia katika michuano ya kombe la Kagame na alifanya vizuri zaidi ya wachezaji aliowakuta
Baada ya kambi ya siku 11 nchini Morocco, matarajio ni kuwa mwelekeo wa Yanga mpya utaanza kuonekana
August 29 siku ya kilele cha wiki ya Mwananchi, mashabiki watakuwa na nafasi ya kushuhudia burudani kutoka kwa timu yao iliyosukwa upya