Kiungo Mganda Halid Aucho anahusishwa na miamba wa soka nchini Yanga na Simba
Aucho kwa sasa yuko kwao Uganda akirejea kutoka hapa Tanzania ambapo alifanya mazungumzo na Simba kisha Yanga
Inaelezwa kiungo huyo alikuja kwa mwaliko wa Simba, lakini Yanga walipata nafasi ya kuzungumza nae pia
Pamoja na mahitaji yake makubwa ya Mshahara, Mwenyekiti wa Makampuni ya GSM Ghalib Said Mohammed amekubali mwamba huyo asajiliwe
Akiwa kwao Uganda, Aucho amethibitisha ni kweli alikuwa Tanzania lakini hakutaka kuweka wazi ni timu ipi amemalizana nayo akisema klabu ndio yenye jukumu la kutangaza usajili wake
Taarifa zisizo na shaka kutoka ndani ya uongozi wa Yanga, zimebainisha kuwa GSM wametoa 'mkwanja' kukamilisha usajili wake
Katika mapendekezo ya usajili ambayo kocha Nasreddine Nabi aliwaachia viongozi wa Yanga ni pamoja na usajili wa viungo wawili, mmoja mkabaji na mwingine wa ushambuliaji
Aucho ni kiungo mkabaji mwenye uzoefu wa soka la Afrika. Amepata nafasi ya kucheza soka barani Ulaya na ligi zenye ushindani kama Misri na Afrika Kusini. Ni mchezaji tegemeo wa timu ya Taifa ya Uganda
Yanga ikiwa inaenda kushiriki michuano ya ligi ya mabingwa, inahitaji wachezaji aina ya Aucho katika kukiimarisha kikosi chake
Huyu ni mchezaji ambae wengi wanatamani kumuona akiivaa uzi wa njano na kijani msimu ujao, bila shaka wikiendi hii itafahamika