Msimu umemalizika mkoani Kigoma jana kwa Yanga kupoteza mchezo wa fainali kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya watani zao Simba kwa kufungwa bao 1-0
Hayakuwa ni matokeo ambayo Wanayanga walitamani kuyapata, lakini ndivyo mpira wa miguu ulivyo, matokeo ni aina tatu, utashinda, utafungwa au utatoka sare
Jambo la kujivunia kwa Yanga ni vile wachezaji walivyomaliza msimu kwa kuipigania timu licha ya kucheza nusu ya mchezo wakiwa pungufu kutokana na kadi nyekundu aliyopewa kiungo Mukoko Tonombe
Kwa hakika hakuna mchezaji anaweza kulaumiwa kwa vile walivyojitoa katika mchezo huo. Ni matokeo tu, yamepita na sasa fikra zinapaswa kuelekea maandalizi ya msimu ujao
Ni wazi baadhi ya wachezaji watapewa mapumziko ya siku chache kabla ya kurejea kambini kwa ajili ya maandalizi ili kushiriki michuano ya kombe la Kagame inayoanza wiki ijayo jijini Dar es salaam
Michuano hii ni muhimu kwa Yanga kwani itawasaidia katika maandalizi kuelekea msimu ujao
Kwa miaka mitatu Yanga haikushiriki michuano hiii sababu ikielezwa ni kuwapa wachezaji mapumziko baada ya msimu kumalizika. Ni msimu uliopita pekee michuano haikufanyika kutokana na janga la corona
Hata hivyo kutokana na ufinyu wa muda kuelekea kuanza kwa msimu ujao, yangekuwa ni makosa makubwa kutoshiriki wakati huu
Yanga itasajili wachezaji wapya, michuano hii inaweza kumsaidia kocha Nasreddine Nabi kupata muunganiko wa nyota wapya na wale watakaoendelea kubaki
Ifahamike Yanga itashiriki michuano ya ligi ya mabingwa msimu ujao ambayo inaanza mwanzoni mwa mwezi Septemba 2021
Hivyo kuna takribani wiki sita za maandalizi kabla ya kuanza michuano hiyo
Ligi Kuu msimu wa 2021/22 nayo itaanza Septemba wiki moja kabla kutakuwa na mchezo wa Ngao ya Jamii dhidi ya Simba hivyo hakuna muda zaidi