Hatimaye Julai 25 imewadia Wananchi! Ile siku iliyokuwa ikizungumzwa zaidi na mashabiki wa soka nchini imewadia!
Ni siku ya mtanange mwingine wa kihistoria kati ya watani wa jadi Yanga na Simba, sasa ukipigwa kule mkoani Kigomaa
Ni mchezo wa fainali kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) ambao unakwenda kuingia katika historia ya klabu hizo kongwe zaidi nchini
Ni mchezo wa pili baina ya timu hizo mwezi huu. Julai 03 kilipigwa pale uwanja wa Benjamin Mkapa katika mchezo wa ligi kuu na Wananchi wakaondoka na ushindi wa bao 1-0 wakizima tambo za watani zao Simba waliokuwa wakiamini ingekwa rahisi kwao kuondoka na alama zote tatu mbele ya Yanga
Ni mchezo wa tatu baina ya timu hizo mwaka huu, kwani inakumbukwa mwezi Januari walikutana kule visiwani Zanzibar katika mchezo wa fainali kombe la Mapinduzi ambapo Wananchi waliondoka na kombe baada ya kuibuka na ushindi kupitia mikwaju ya penati
Leo Yanga wanasaka ushindi wa tatu mfululizo dhidi ya watani zao mwaka huu. Lakini ushindi wa leo utakuwa muhimu zaidi kwani pamoja na furaha ya kumfunga mtani, wataondoka na kombe uwanjani
Kwa Simba, watajaribu kujitutumua kufuta uteja mbele ya Yanga. Msimu uliopita katika michuano hii, Simba walipata ushindi wa mabao 4-1 katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Yanga ambao ulipigwa uwanja wa Benjamin Mkapa
Lakini leo ni mchezo mwingine, unaopigwa mkoani Kigoma, hukooooo mwisho wa reli
Mji wa Kigoma umefurika! Wananchi kutoka kila pembe ya Tanzania wako Kigoma wakisubiri mtanange huo utakaounguruma kuanzia saa kumi jioni
Ni mchezo mwingine mgumu ambao dakika 90 ndizo zitakazotoa majibu ya nani ataondoka na taji la FA
Kwa Yanga ni muhimu kushinda ili kumaliza msimu na kombe. Pamoja na kuwa walishinda taji la Mapinduzi, kushinda FA ni heshima kubwa zaidi
Ari na morali ya vijana wa Kocha Nasreddine Nabi iko juu, kwao hii ni vita ambayo wanapaswa kuishinda
Wenyewe wanasema afe kipa, afe beki lazima Mnyama achinjwe leo na kombe kuelekea viunga vya Jangwani
Ni saa kumi jioni ya leo pale uwanja wa Lake Tangayika. Kila la kheri Wananchi