Pamoja na kuwa Yanga tayari imejihakikishia nafasi ya kushiriki michuano ya CAF msimu ujao, Wananchi wamesisitiza kuwa watahakikisha wanashinda mchezo wa fainali kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Simba ambao utapigwa Jumapili, Julai 25 uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma
Yanga imewasili Kigoma mapema leo kukamilisha maandalizi yake ya mwisho kabla ya kuwakabili watani zao katika mchezo ambao kombe litakuwa uwanjani
Afisa Mhamasishaji wa Yanga, Antonio Nugaz amesema timu iko imara na wako Kigoma kwa kazi moja tu, kutwaa ubingwa wa michuano hiyo
Nugaz amesema wanahitaji ushindi dhidi ya watani zao ili kujitwalia tiketi ya kushiriki mashindano ya CAF kwa nguvu zao
"Sisi tumejiandaa kikamilifu na tumekuja Kigoma kwa kazi moja tu, kuifunga Simba na kuwa mabingwa wa FA. Tunataka kwenda Kimataifa kwa nguvu zetu, tukutane Lake Tangayika siku ya Jumapili" alitamba Nugaz

Naye mfungaji bao pekee la Yanga katika mchezo wa ligi uliopigwa Julai 03, Zawadi Mauya amesema wamefanya maandalizi ya kutosha na wako tayari kuwapa furaha mashabiki wao katika mchezo huo
"Sisi wachezaji tumejiandaa tuko vizuri, nawaambia mashabiki watarajie mambo makubwa kutoka kwetu kwani tumejiandaa kupata ushindi," alisema Mauya
Yanga imetua mkoani Kigoma ikiwa na msafara wa wachezaji 20, benchi la ufundi na waandamizi wakiongozwaMwenyekiti Dk Mshindo Msolla, Kaimu Katibu Mkuu Haji Mfikirwa na Makamu Mwenyekiti wa kamati ya Mashindano Injinia Hersi Said