Naona huu mjadala wa tetesi za usajili zinazomuhusu kiungo Ibrahim Ajibu umeendelea kuumiza vichwa vya Wanayanga wakigawanyika makundi mawili
Wapo wanaunga mkono kurejeshwa kwa kiungo huyo lakini wengine wanasema hawataki kumuona
Lakini mwisho wa siku naamini usajili unafanywa kwa kuzingatia mahitaji ya timu na sio matakwa ya mtu mmoja mmoja
Kama benchi la ufundi litaona inafaa kumsajili Ajibu nadhani haitakuwa vyema mashabiki kupinga kwani mwisho wa siku wao wanahitaji furaha tu
Ajibu ni mchezaji mzuri na alifanya vizuri sana wakati anaitumikia Yanga msimu wa 2018/19
Katika msimu huo, Ajibu aliweza kutengeneza mabao 24, kafunga saba na kutoa pasi 17 za mabao
Wakati huo Yanga haikuwa sawa lakini alishirikiana vyema na kina Heritier Makambo na nyota wengine kuwapa furaha mashabiki katika kipindi kigumu cha ukata
Ni nyakati ambazo Ajibu alikuwa katika ubora hasa. Wananchi walimuamini sana, akapewa unahodha wa timu na zaidi akachaguliwa kuwa mmoja wa watia saini wa akaunti iliyokuwa imefunguliwa kwa ajili ya kuichangia Yanga
Aliamua kurudi Simba kufuata pesa bila ya kujali thamani ambayo Wananchi walimpatia, hilo ndilo linalowaumiza wengi
Lakini wakati mwingine mchezaji yeyote anaweza kufanya maamuzi kama yake. Yanga haikuwa na pesa wakati ule, uhakika wa kulipa mishahara haukuwepo
Ilikuwa sio rahisi kumshawishi asaini mkataba mpya wakati anafahamu hatakuwa na uhakika wa kulipwa kila mwezi
Sio Ajibu tu, wachezaji wengi wazuri hawakuwa tayari kujiunga na Yanga wakati ule kwa sababu walifahamu kuna changamoto katika ulipaji wa mishahara
Yanga sasa imetoka huko, 'fedhwa ipo' na ndio maana amerudi kuomba arejeshwe kundini kwani anafahamu heshima yake aliipatia Yanga
Hata hivyo, anayepaswa kuamua usajili ni kocha Nasreddine Nabi, lakini kama usajili wa Ajibu sio matakwa ya benchi lake la ufundi, basi hautakuwa na umuhimu