Pamoja na dirisha la usajili kufunguliwa hapo jana, kwa sasa uongozi wa Yanga umeelekeza nguvu kwenye mchezo wa fainali ya kombe la Shirikisho la Azam (ASFC) dhidi ya Simba ambao utapigwa Jumapili, Julai 25 uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema tayari wamepokea mapendekezo ya usajili kutoka kwa kocha Nasreddine Nabi na wameanza mazungumzo na baadhi ya wachezaji hao
Amesema michakato ya usajili itawekwa hadharani baada ya mchezo dhidi ya Simba
"Tumekusudia kufanya maboresho katika maeneo ambayo kocha amependekeza tuyafanyie kazi. Mazungumzo na baadhi ya wachezaji yanaendelea. Baada ya mchezo wa fainali ya FA, tunaweka hadharani wachezaji tuliowasajili"
"Msimu huu tutakuwa na utaratibu tofauti wa utambulisho. Yanga imejaa viongozi wabunifu, msimu uliopita tulikuwa na utaratibu wake na msimu huu mtarajie utaratibu tofauti," alisema Bumbuli
Mashabiki wa Yanga wanasubiri kuona maboresho yaliyofanywa ili kuhakikisha msimu ujao mabingwa hao wa kihistoria wanaurejesha ubingwa Jangwani baada ya kuukosa kwa misimu minne