Siku ya jana iliandikwa historia baada ya Yanga Sc na Azam Media kusaini Mkataba wa makubaliano ya haki za maudhui wenye thamani ya Bilioni 41 pamoja na VAT
Ilikuwa siku ya furaha kwa Wananchi ambao katika kipindi cha misimu minne wameikosa furaha hiyo kutokana na klabu yao kupitia katika changamoto za kiuchumi
Shukrani kwa GSM ambao tangu walipoanza kuisaidia Yanga mwezi Novemba 2019, wameweza kuirejesha timu katika mazingira bora ukilinganisha na ilivyokuwa mwanzo
Jambo moja kubwa baada ya kusaini mkataba huo, kuanzia msimu ujao, Yanga ina uhakika wa kulipa mishahara ya wachezaji kupitia fedha za Azam kwani kila mwezi watapokea Tsh Milioni 200 fedha ambazo zitakuwa na ongezeko kila mwaka katika kipindi chote cha miaka 10 ya mkataba
Fedha hizi ni nje ya fedha za haki za matangazo ya televisheni ambazo watazipokea kutoka Azam Media kama ilivyo kwa klabu zote za Ligi Kuu
Aidha, neema hii imekuja kipindi ambacho Yanga iko katika mchakato wa kuingia kwenye mabadiliko baada ya kubadili mfumo wake wa uendeshaji
Tutarajie Mabilionea wengine kujitokeza kununua hisa asilimia 49% za kampuni ya Yanga ambazo zitawekwa sokoni baada ya mchakato kukamilka
Hii ina maana Yanga itakuwa na msuli mpana wa kiuchumi pengine kuliko klabu yoyote hapa Tanzania
Kuna mabilioni ya Azam Media ambapo Wananchi watakusanya zaidi ya Bilioni 3 kwa mwaka kama watamaliza nafasi mbili za juu kwenye msimamo wa ligi, Mabilioni yatakayoletwa na Wawekezaji, Wadhamini, ada za mashabiki na Wanachama na viingilio milangoni ni sehemu ya fedha ambazo Yanga watakusanya
Hapa Mwenyekiti wa Yanga Dk Mshindo Msolla anastahili pongezi kwa kuwa chachu ya kufanikishwa haya
Kama sio utashi wa uongozi wake, pengine mengi yasingewezekana. Yeye na viongozi wenzake pale Yanga bila kuwasahau wadhamini GSM wamekuwa na mchango mkubwa katika kubadili mtazamo wa wadau wa Yanga na hatimaye kufanya Mabadiliko muhimu ambayo matunda yake yameanza kuonekana