Kuelekea mchezo dhidi ya Simba baadae leo, kocha mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi wala haumizi kichwa kwani majembe yake yako tayari kwa mchezo huo
Ni wachezaji watano ambao hawatakuwa sehemu ya mchezo siku ya leo Lamine Moro, Michael Sarpong, Haruna Niyonzima, Metacha Mnata, na Mapinduzi Balama
Ukimuondoa Balama ambaye bado hajaanza mazoezi ya timu, Lamine, Sarpong na Niyonzima hawakuwa kwenye mpango wa Nabi kwa takribani michezo minne kutokana na majeruhi na sababu za kinidhamu
Aidha mlinda lango Metacha Mnata amefungiwa na TFF kutokana na tukio la utovu wa nidhamu alilofanya baada ya mchezo dhidi ya Ruvu Shooting
Metacha pia amesimamishwa na uongozi wa Yanga kwa muda usiojulikana
Jambo jema zaidi ni kuwa Nabi tayari ameshapata kikosi chake cha kwanza ambacho bila shaka leo hakitakuwa na mabadiliko makubwa
Langoni yupo Farouk Shikhalo wakati kwenye safu ya ulinzi wako Kibwana Shomari, Adeyum Saleh, Dickson Job na Bakari Nondo Mwamnyeto
Kurejea kwa Yassin Mustafa na Abdallah Shaibu 'Ninja' pengine kunaweza kupelekea mabadiliko ingawa sio jambo linalotarajiwa sana kwani nyota hao walikuwa nje kwa takribani wiki nane na walianza mazoezi mwanzoni mwa wiki hii
Eneo la kiungo Nabi amewatumia Mukoko Tonombe na Zawadi Mauya katika michezo iliyopita huku akimsogeza Feisal Salum 'Fei Toto' mbele yao
Katika mchezo wa leo huenda akamuhitaji Saido Ntibazonkiza kuanza na hivyo anaweza kumrejesha Feisal nafasi ya Mauya na Antibiotic kucheza namba 10
Deus Kaseke, Tuisila Kisinda wanashambulia wakitokea pembeni wakati Yacouba akiwa mshambuliaji wa kati
Nabi anapendelea zaidi kutumia mfumo wa 4-2-3-1 na ndio ulimpa matokeo ya ushindi katika michezo mitano iliyopita
Hiki ndicho kikosi cha Nabi ambacho kimetengeneza muunganiko, wakicheza kwa maelewano mazuri katika michezo iliyopita ambapo wameweza kushinda michezo mitano mfululizo