Aliyekuwa Kocha Mkuu wa timu ya Wanawake ya Yanga Princess Edna Lema huenda akaachana na mpango wa kuondoka baada ya kikao na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Injinia Hersi Said ambaye ni Mkurugenzi wa Uwekezaji kampuni ya GSM
Katika kikao hicho, Injinia Hersi alieleza kutoafiki uamuzi wa Edna kuondoka Yanga Princess hasa kutokana na kazi nzuri aliyofanya katika misimu miwili
"Msimu wako wa kwanza Yanga Princess ilimaliza katika nafasi ya nane lakini kwenye msimu wako wa pili ilibaki alama moja tu uweze kuchukua ubingwa. Kwangu mimi ulistahili kabisa kushinda ubingwa, ni bahati mbaya tu jambo hilo halikutokea," alisema Hersi
"Lakini pia umejenga mahusiano mazuri na wachezaji klabuni na hata kwenye timu ya Taifa ambako wewe ni kocha msaidizi, kwa kweli hili ni jambo ambalo unapaswa kulifkiria upya kwani kama ni suala la maslahi tunaweza kuzungumza na tukafikia mwafaka"
"Nina imani kubwa tukiwa nawe msimu ujao, na kwa kikosi hiki ambacho umekijenga, tutashinda ubingwa"
Lema ameyapokea mapendekezo hayo ya Yanga na kukiri kuwa anahitaji kufikiri machungu wanayopata wachezaji wake baada ya kupata taarifa kuwa hatakuwa nao msimu ujao
"Nimepokea meseji na ujumbe kutoka kwa wachezaji wakihuzunika baada ya kusikia mimi naondoka. Naambiwa baadhi ya wachezaji jambo hili limeathiri hata maisha yao hivyo nadhani napaswa kufikia upya uamuzi niliochukua awali," alisema Lema
Inaelezwa Lema alikuwa mbioni kujiunga na timu ya Wanawake ya Zesco nchini Zambia lakini ni wazi baada ya kikao hicho, anaweza kuendelea kuinoa Yanga Princess