Keshokutwa Jumamosi dabi ya Kariakoo itaunguruma pale uwanja wa Benjamin Mkapa wakati Wananchi watakaposhuka dimbani kuwakabili watani zao Simba katika mchezo ambao wao watakuwa wageni
Ni mchezo wa pili wa ligi msimu huu, kumbukumbu za mchezo wa duru ya kwanza matokeo yakiwa sare ya bao 1-1
Awali mchezo huo ulipaswa kupigwa May 08 lakini ukabadilishwa muda na baadae kusogezwa mbele katika mazingira ya kutatanisha
Lakini hatimaye Wananchi wamesamehe yaliyotokea na sasa wanakwenda kudhihirisha kuwa wao wako tayari kucheza na Simba wakati wowote
Kikosi cha Kocha Nasreddine Nabi kimeimarika sana ukilinganisha na kile kikosi cha Cedric Kaze ilichocheza mchezo wa duru ya kwanza
Wananchi sasa wanacheza kwa malengo na mipango inaonekana na muhimu zaidi ni ubora wa wachezaji
Mashabiki wamekuwa wakiaminishwa kuwa Simba ndio timu yenye wachezaji bora zaidi, Yanga ina wachezaji bora na hatari
Kikosi cha Nabi 'kimesimama', wameshinda mechi tano zilizopita katika mashindano yote
Unazungumzia timu yenye mshambuliaji kama Yacouba Songne ambaye amepachika mabao 10 katika mashindano yote
Kila mmoja anafahamu timu ilikuwa na changamoto kwenye eneo la ushambuliaji, lakini tangu alipotua Nabi, Yacouba amekuwa na rekodi nzuri ya kuzifumania nyavu, kwa wastani anafunga kwenye kila mchezo
Wapo kina Deus Kaseke ambao majina yao hayatajwi sana pengine kwa sababu ni mchezaji wa ndani. Kaseke ameweka kambani mabao nane katika mashindano yote na kutoa pasi sita za mabao
Pale eneo la kiungo kuna mtu anaitwa Mukoko Tonombe, Mcongomani huyu yuko kwenye kikosi cha timu ya Taifa ya DR Congo na anacheza huko
DR Congo ina zaidi ya wachezaji 100 wanaosakata kabumbu ligi za Ulaya, kuitwa na kupata namba kwenye timu hii ya Taifa sio jambo dogo
Mukoko ndiye aliyeibuka nyota wa mchezo wa duru ya kwanza uliomalizika kwa sare ya bao 1-1
Hivi unawezaje kumbeza mchezaji kama Feisal Salum 'Fei Toto'? Huyu kwa sasa ndio roho ya timu ya Taifa ya Tanzania. Mechi za karibuni ameonyesha ni hatari akitumika kama namba 10 kwani amefunga, amesababisha penati na kutoa assisti
Safu ya ulinzi kuna mtu anaitwa Dickson Job, kwa wasiomfahamu huyu wamuulize kocha wa timu ya Taifa Kim Poulsen
Nahodha Bakari Nondo Mwamnyeto ameendelea kudhihirisha thamani yake, huyu ndio beki ghali zaidi kwa wachezaji wa ndani
Lakini pia Abdallah Shaibu Ninja nae amerejea baada ya kupona majeraha kama ilivyo kwa Yassin Mustafa
Huyu Ninja, Kagere na Mugalu wanaikumbuka shughuli yake Mapinduzi Cup kule visiwani Zanzibar
Siku hiyo Simba ilipata 0 shoot on target, sababu ya ukuta wa chuma ulioongozwa na Ninja akisaidiana na Said Juma Makapu, Adeyum Saleh, Kibwana Shomari bila ya kumsahau mlinda lango Faruk Shikhalo
Tuisila Kisinda, ameshawaadhibu hata kabla ya kuja Tanzania wakati yuko AS Vita. Huyu najua hawataki kumsikia kwani wanafahamu kwa ukuta wao ule labda TFF wawaruhusu mabeki wao wacheze na 'Bodaboda'
Saido Ntibazonkiza, mchezaji wa mechi kubwa, huu utakuwa mchezo wake wa pili wa dabi. Hivi unawezaje kumbeza mchezaji aliyecheza ligi kuu kule Ufaransa na Ubelgiji? Huyu Saido ni mchezaji wa daraja la juu kabisa ambaye Simba hawana
Ana mabao manne na assist tano akiwa amecheza chini ya mechi 10 za ligi kwenye kikosi cha Yanga
Kiufupi Wananchi wako tayari, Jumamosi watajua hawajui! Muhimu wasije na matokeo mfukoni waache dakika 90 ziamue,