Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano klabu ya Yanga Hassan Bumbuli amewata mashabiki wa timu hiyo kutokuwa na hofu yoyote kuelekea mchezo wa ligi dhidi ya Simba ambao utapigwa siku ya Jumamosi, Julai 03 katika uwanja wa Benjamin Mkapa
Baada ya msemaji wa Simba Haji Manara kutamba kuwa timu yao ina wachezaji wazuri na haiwezi kufungwa na kikundi cha watu, Bumbuli amesema kuzungumza ni kawaida yao lakini matokeo ya uwanjani huwa tofauti
"Sisi tupo tayari kwa mchezo wa Jumamosi, kuna watu wanajisifu wana wachezaji wazuri wa dunia nzima lakini tumekutana nao mara tatu kwenye ligi hawajatufunga na mara ya mwisho walichomoa dakika za majeruhi"
"Kikubwa nawaambia mashabiki wa Yanga mjitokeze kwa wingi tena wala msiwe na hofu. Waambieni waje uwanjani," alitamba Bumbuli
Yanga itaingia katika mchezo huo wa Jumamosi ikiwa na takwimu nzuri za matokeo dhidi ya watani zao Simba katika michezo mitano iliyopita
Ushindi mechi mbili, sare mechi mbili na kupoteza mchezo mmoja