Rais mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania awamu ya nne Dk Jakaya Kikwete amewapongeza Wanachama wa klabu ya Yanga kwa kufanya marekebisho ya katiba ambayo yataruhusu Mabadiliko ya mfumo wa Uendeshaji
Dk Kikwete ambaye alikuwa mgeni rasmi wa Mkutano huo, amesema baada ya Mabadiliko hayo, hatarajii kuona vikundi vya watu wakipingana huko nje
Amesema Wanachama wamepata nafasi ya kuhoji na kujadiliana kabla ya zoezi hilo kuhitimishwa leo
"Mashabiki wa Yanga wakosoe kwa nia ya kujenga na sio kukosoa kwa lengo la kukomoa. Msiache kusema kwenye mkutano mkuu halafu mnaenda kulalamika vijweni. Huo ni usengenyaji. Watu wa namna hii waambieni, acheni uchimvi. Usianzishe ligi mtaani mnabomoa klabu yenu," alisema Dk Kikwete
Aidha Dk Kikwete amewataka Wanachama wa Yanga waendelee na utamaduni wa kuhoji masuala ya fedha ndani ya klabu yao ili kuhakikisha viongozi wanawajibika katika matumizi ya fedha
"Waulizeni viongozi kuhusu hesabu za klabu yenu wasiishie kuwaambia unajua hii klabu tunaendesha kwa hasara, kiongozi asijimilikishe klabu ana wajibu kwa waliomchagua"
"Iliwahi kupita kipindi Yanga haina ukaguzi wa kifedha. Lakini sasa hivi Yanga inaendeshwa kisasa. Hesabu zao zinakaguliwa na wakaguzi wanaotambulika na serikali na sio makanjanja. Wizi unapungua na udokozi unapungua. Kuna watu waligeuza vilabu kuwa MKUKUTA wake"
Dk Kikwete pia amesisitiza klabu kuwekeza kuijenga timu kuliko kuendeleza mambo ya kamati za ufundi ambayo hayana manufaa kwa klabu
"Lipeni wachezaji vizuri na kwa wakati. Hii inapunguza klabu kutegemea zaidi kamati za ufundi kuliko benchi la ufundi. Klabu ikiendekeza sana kamati za ufundi haiwezi kupiga hatua"
Dk Kikwete amesema Wanachama leo wamefanya uamuzi sahihi wa kukubali muundo uliopendekezwa ambao utapelekea klabu kuendelea kubaki mikononi mwao
"Mwekezaji asigeuzwe kuwa mmiliki wa klabu. Hii ni klabu ya wanachama. Mwekezaji anakuja kujumuika na wenye klabu yao kusogeza klabu mbele kibiashara na sio kujimilikishia klabu. Nilichovutiwa na Yanga mabadiliko haya ni shirikishi. Yamejadiliwa na maoni yamepokelewa"