Muda kama huu wiki ijayo, Juni 27 2021 Wananchi watakuwa wameanza kuzungumza lugha nyingine kuhusu timu yao
Ni kwamba siku hiyo Wanachama wa Yanga wataamua kufungua ukurasa mpya kwa timu yao au wabakie katika zama zilezile za machungu
Ni Mkutano Mkuu wa Wanachama ambao utaweka historia kwa kupitisha au kukwamisha ajenda muhimu inayobeba hatma ya klabu yao
Kwa miaka 86 Yanga imemilikiwa na Wanachama kwa asilimia 100. Lakini umefika wakati Wananchi wanahitaji kujaribu muundo mwingine ambao utawaongezea nguvu za kiuchumi
Wanachama wataendelea kuwa wamiliki wa klabu kwa kuhodhi asilimia 51 ya hisa huku wawekezaji wakinunua asilimia 49
Wawekezaji watakuwa na jukumu la kusimamia masuala yote ya kifedha pamoja na kiutawala. Huu ndio muundo ambao klabu nyingi zilizofanikiwa zinatumia
Mpira wa sasa ni pesa, tusijidanganye, kama timu haina uwezo wa kiuchumi kwa mpira wa kisasa, mafanikio yatakuja kwa bahati mbaya tu
Ili timu iweze kuwa na mafanikio ya kweli inahitaji viwanja vizuri kwa ajili ya mazoezi, benchi la ufundi, wachezaji wazuri na mazingira bora ya kambi
Haya yote yanahitaji pesa, Wanachama peke yao hawawezi. Yanga imemilikiwa na Wanachama kwa miaka 86 lakini changamoto zimekuwa nyingi
Hivyo Juni 27 ni siku muhimu sana kwa Wanachama wa Yanga, kwa hakika hawapaswi kufanya makosa