Baada ya mapumziko ya takribani wiki tatu, leo Yanga wanarejea dimbani pale kwa Mkapa kuwakabili Ruvu Shooting katika mchezo wa ligi kuu ya Vodacom
Ni moja ya michezo mitano iliyosalia kufunga hesabu za msimu huu kwa upande wa Wananchi
Hautakuwa mchezo mwepesi kutokana na kila timu kuzihitaji alama tatu
Ruvu Shooting wamekuwa na mwenendo wa kusuasua, wanasaka matokeo ili kujiweka katika eneo salama kuepuka kuteremka daraja
Kwa Yanga matokeo tofauti na ushindi yataendelea kuwarahisishia watani zao Simba kuchukua ubingwa
Lakini pia yanaweza kuipa nafasi Azam Fc kusogea kwenye nafasi ya pili kama watashinda mchezo wao dhidi ya Gwambina Fc
Yanga itaingia kwenye mchezo huo ikiwa na kikosi chake kamili, nyota waliokuwa na majukumu ya timu za Taifa wote wamerejea
Akizungumzia maandalizi ya mchezo huo hapo jana, kocha wa makipa Razack Siwa alisema kuwa wametumia vyema kipindi cha mapumziko ya michezo ya Kimataifa kujiimarisha
Alisema wamejipanga kushinda mchezo huo pamoja na michezo mingine iliyobaki ili kubaki katika mbio za ubingwa
Mchezo utapigwa kuanzia saa moja kamili usiku